Na OWM – TAMISEMI
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif, amekutana na wanafunzi zaidi ya 200 wanaosoma Stashahada ya Utabibu katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mafinga, na kutumia fursa hiyo kutoa maelekezo na miongozo muhimu kuhusu maadili ya taaluma ya afya pamoja na wajibu wao kwa jamii.
Akizungumza na wanafunzi hao, Dkt. Jafar amewataka kusoma kwa bidii, kuzingatia maadili ya kitaaluma na kutambua kuwa taaluma ya afya si ajira ya kawaida bali ni wito unaohitaji nidhamu, uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu.
"Tofauti na kada nyingine, wahudumu wa afya wanamhudumia moja kwa moja mgonjwa ambaye jambo la kwanza analohitaji ni huruma.amesema Dkt. Jafar
Amefafanua kuwa mhudumu wa afya aliyepewa dhamana na jamii pamoja na Serikali anapaswa kutambua kuwa mwenendo wake una athari ya moja kwa moja kwa maisha ya wagonjwa na jamii inayomzunguka.
Amehoji kuwa endapo jamii itakosa imani kwa mhudumu wa afya nje ya mazingira ya kazi, itakuwa vigumu kwake kuaminiwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yake hospitalini.
Aidha, Dkt. Jafar amewataka wanafunzi hao kujifunza na kuishi misingi ya upendo na kutumia lugha njema katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
"Kada ya afya ni kada ya huruma, ambapo mhudumu wa afya mwenye upendo husaidia kumpunguzia mgonjwa msongo wa mawazo, hali inayochangia kuboresha afya ya mgonjwa na kuongeza ufanisi wa huduma za afya kwa ujumla. amesisitiza Dkt.Jafar
Amesisitiza kuwa Serikali, kupitia TAMISEMI, inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya kwa usawa, haki na upendo bila ubaguzi wa aina yoyote, na kwamba matarajio ya Serikali ni kuona wahudumu wa afya wanazingatia misingi hiyo katika maeneo yao ya kazi.
Halikadhalika, amewahimiza wanafunzi hao kujiandaa kuwa watumishi wa umma wanaotanguliza maslahi ya wananchi, wakitambua kuwa wao ni sehemu muhimu ya jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.