Na. Faraja Mbise, DODOMA
Kina mama wamepewa elimu ya unyonyeshaji sahihi maziwa ya mama kwa lengo la kuwajengea uelewa mpana utakaowasaidia kuwakuza vizuri watoto wao ili wawe na afya njema na lishe bora katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Hayo yalisemwa na Afisa Muuguzi Msaidizi, Kituo cha Afya Makole, Christopher Tarimo, alipokuwa akitoa elimu ya namna sahihi ya kumnyonyesha mtoto na lishe kwa akina mama waliojifungua katika wodi ya wazazi kituoni hapo.
Akizungumza na akina mama hao Afisa Muuguzi Msaizidi, aliwashauri kuzingatia mikao ya unyonyeshaji pindi wanapowanyonyesha watoto wao. “Katika unyonyeshaji lazima tutenge muda, ile nusu saa ya kwanza au lisaa limoja hakikisha kwamba simu umeweka pembeni, hausumbuliwi na mtu yeyote unakuwa umetulia mawazo yote kwa mtoto. Unatakiwa uwe umekaa, tunashauri sana kumnyonyesha mtoto ukiwa umekaa, hakikisha umekaa mkao ambao upo ‘comfortable’ kwamba umeridhika, mgongo wako umekaa sehemu ambapo hautadondoka, hakikisha kichwa cha mtoto wako kipo kwenye kiwiko, hakikisha tumbo la mtoto na lako yanatazamana na unahakikisha mtoto anakuangalia na wewe unamuangalia usoni. Kwasababu gani tunasema hivyo, ili uweze kuona ameshika chuchu vizuri, uwe makini je, mtoto kapaliwa, au mtoto anasinzia” alishauri kwa msisitizo Tarimo.Akiongelea ushikaji sahihio wa mtoto wakati wa kunyonyesha alisema kuwa ili mtoto anyonye vizuri anatakiwa kushikwa vizuri asiweze kupaliwa na maziwa na kumfanya ashindwe kunyonya.
“Ukimnyonyesha mtoto hakikisha vidole vinne vinakuwa chini ya titi na ile alama nyeusi ya chuchu yote inazama mdomoni. Chuchu ikizama mdomoni hautosikia sauti kama ya mguno, usiposikia hiyo sauti hapo mtoto wako ananyonya vizuri na hanyonyi hewa. Na hakikisha kwenye ziwa moja, mtoto ananyonya si chini ya dakika 30. Tunasema hivyo, kwa sababu maziwa yamegawanyika, kuna maziwa ya mwanzo, kati na mwisho. Kwahiyo, ukimnyonyesha ndani ya dakika 10 na ukamtoa atakuwa amenyonya maji, yale maziwa yenye virutubisho hatoyapata” alisema Tarimo.
Vilevile, alikwakumbusha akina mama kuzingatia mlo kamili ili kumkinga mtoto na magonjwa yatokanayo na lishe duni kama udumavu wa mwili na akili, uzito kupita kiasi na ukondefu.
“Naomba niwakumbushe swala zima la mlo, mtoto anakula kupitia mama, yaani wewe usipokula mtoto nae hali. Kwasababu, kile unachokula ndicho kinachoenda kumeng’enywa ndani ya mwili, baadhi kinachukuliwa kinapelekwa kwenye maziwa. Kwahiyo, hakikisha unapokula milo yako asubuhi, mchana na jioni, hiyo milo iwe ya kukusaidia wewe kupata virutubisho kwa mtoto” alisisitiza Tarimo.
Kwa upande wake Gladness Mauki, mkazi wa Chidachi alisema amefurahishwa kukutana na mafunzo hayo ya lishe kwa mtoto na mikao sahihi ya kumnyonyesha pia kwasababu hakutegemea. Alitoa rai kwa akina baba kuwa mstari wa mbele kuwasaidia kina mama katika kukumbushana namna sahihi ya kutoa malezi bora kwa mtoto. “Leo nimekuja kliniki, sikujiandaa kukuta mafunzo yaliyokuwa yanaendelea, nimeshangaa tu kukuta akina mama wengi. Sana sana nimejifunza mtoto anatakiwa kuanza kula chakula mara baada ya kufikisha miezi sita lakini nimejifunza anapofikisha hiyo miezi sita, sio lazima kumpa mtoto chakula kingi hapo mwanzoni ila unaweza kumpa mtoto chakula taratibu. Pia nimejifunza namna nzuri ya kumnyonyesha mtoto, muda ambao mtoto anatakiwa kunyonya uwe ni kiasi gani. Napenda niwashukuru kwa kutoa huduma hii na niwashauri pia watoa mafunzo wasiache kuja mara kwa mara maana tunapata mafunzo yanayotusaidia katika malezi ya watoto. Pia akina baba wasiache kuwasindikiza kina mama kuja kliniki ili kuweza kuwa ‘support Psychologically’ kutoa msaada wa hapa na pale, baba anaweza akawa ni mtu wa karibu atakayeweza kumpatia msaada mkewake” alisema Mauki.
Nae Kurwa Kajoro, mkazi wa Michese alitoa rai kwa akina baba wenzake kuhudhuria kliniki na akina mama ili nao waweze kuelewa kinachoendelea na kuweza kuwakumbusha kina mama katika utekelezaji wa malezi bora kwa watoto. “Wito wangu kwa kina baba, ninaposema kliniki ya mama, baba na mtoto ni muhimu kwa wazazi wote sio kwamba tunamuachia anakuja mama tu. Mfano, kwa mafunzo tuliyoyapata leo kwa wataalamu kutoka Kituo cha Afya Makole, ni kwamba tunaweza kusaidia, mama anapokuwa amesahau yale ambayo umeyasikia unaweza kumkumbusha na kufanya mkawa na malezi bora kwa watoto” alisisitiza Kajoro.
Maziwa ya mama ni lishe bora kwa mtoto, hivyo kunyonyesha sio tu husaidia kuwa na mahusiano mazuri kati ya mama na mtoto bali ni manufaa kwa afya ya mama yakitajwa kuwa na faida kadha zikiwa ni pamoja na maziwa kuwa kiungo muhimu kwa maendeleo ya afya, virutubisho bora kwa mtoto anayekua, kumsaidia kujikinga dhidi ya magonjwa, kuzuia unene wa kupindukia utotoni na kuongeza uwezo wa utendaji kazi wa ubongo na kupunguza hatari ya kansa na magonjwa mengine.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.